Tunapouanza mwaka 2024, tunaiomba Serikali, wadau mbalimbali na jamii kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kupunguza vitendo vya udhalilishaji ambavyo vinawaathiri zaidi wanawake na watoto, na pia vijana wa kiume ambao takwimu zimekua zikionesha kuwa ndio watendaji wakubwa wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Ripoti ya takwimu za udhalilishaji wa kijinsia kwa mwaka 2023 iliyotolewa hivi karibuni na Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, imeonesha kuwa jumla ya matukio 1954 yameripotiwa kwa mwaka 2023 ambapo kuna ongezeko la matukio 594 ikilinganishwa na matukio 1360 ya mwaka 2022.
Takwimu hizo zinaeleza kuwa kundi kubwa la vijana wa kiume kati ya umri wa miaka 18-29 wameonekana kuwa ndio watuhumiwa wakubwa wa malalamiko hayo ya udhalilishaji ambapo miongoni mwa wanafunzi wa chuo cha mafunzo 111 idadi ya vijana ni 69 ambayo ni sawa na asilimia 62.
Wadau hao wakiongozwa na Serikali wanahitaji kufanya uchambuzi wa kina kujua tatizo la ongezeko hilo, kutoa elimu kwa jamii na kufuatilia matukio yote yanayojitokeza.
Wadau pia wanatakiwa kufuatilia kila hatua inayochukuliwa na jamii, kuripoti malalamiko hayo pamoja na kwenye vyombo vya sheria ili kuhakikisha upatikanaji wa haki, uwazi na uwajibikaji.
Kwa umuhimu wa pekee wadau wanahitaji kutoa elimu kwa vijana kwa kuanzisha kampeni ya kujitambua, kubadilisha tabia na stadi za maisha ambazo zitasaidia kupata ufahamu juu ya madhara ya udhalilishaji na jinsi ya kuzuia.
Watoa mafunzo kwa jamii wakiwemo walimu na wafanyakazi wa afya wanahitaji kuwa na muongozo maalumu utakaoonesha mpangilio wa kutoa elimu, kuonesha viashiria, pamoja na hatua za kuchukua kwa pamoja ili kutokomeza vitendo hivyo.
Tunawaomba wananchi wote, wadau, na jamii kwa ujumla kuungana pamoja katika kupinga vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia, na kuchukua jukumu la kulea na kulinda wanawake na watoto ili kuweza kuwa na taifa bora linalothamini haki za binadamu na usawa wa kijinsia kwa maendeleo ya wote.
Dkt. Mzuri Issa
Mkurugenzi,
TAMWA ZNZ.