Waandishi wa habari wana haki ya kupata taarifa na kuhoji baadhi ya mambo ambayo ni vikwazo vinavyowakabili wao na jamii kwa ujumla kwa lengo la kuleta mabadiliko na maendeleo endelevu katika nchi.
Mkurugenzi wa Chama cha waandishi wa habari Tanzania Zanzibar (TAMWA- ZNZ) Dkt. Mzuri Issa, ameyasema hayo katika mafunzo ya siku mbili ya waandishi wa habari, kuhusiana na utetezi wa mapitio ya sheria za habari yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano TAMWA-ZNZ Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa mwandishi wa habari hunyimwa taarifa na baadhi ya viongozi wa serikali kutokana na maslahi yao binafsi jambo ambalo linakiuka misingi ya Katiba ya nchi na linaminya uhuru wa habari nchini.
‘’hatuna sheria nzuri ya habari inayomwezesha muandishi wa habari kupata habari anayoitaka bila kupata vikwazo, mfano mhusika anapofuatwa na waandishi wa habari kupata maelezo ya jambo fulani basi hujibu tu ahhh!! siwezi kutoa maelezo kwa sasa nitatoa taarifa rasmi kwenye mkutano wa waandishi wa habari (Press conference) hii sio sahihi”, alieleza Dkt Mzuri.
Aidha Dkt. Mzuri amesisitiza kuwa jukumu la waandishi ni kuwajibika kwa jamii na sio kwa viongozi wa serikali au siasa hivyo ni vyema kubadilika na kuzitetea haki zao kwa maendeleo ya tasnia ya hio.
Nae muwezeshaji wa mafunzo hayo Hawra Shamte ambae pia ni mjumbe wa Bodi TAMWA-ZNZ amesema sheria za habari Zanzibar zina mapungufu mengi na ndio maana tunahitaji kupata sheria mpya ya habari itakayoimarisha uhuru wa kujieleza na kupata taarifa.
‘’Endapo tutapata sheria inayokwenda na wakati waandishi tutakuwa huru kupata taarifa na kuandika habari zinazopelekea kukuza maendeleo ya nchi kwa kuibua changamoto mbali mbali zilizomo katika jamii”, Bi Hawra alifafanua zaidi.
Washiriki wa mafunzo hayo wamesemawa wamekuwa wakipata changamoto nyingi katika kuandika habari zenye maslahi kwa jamii na zile za uchunguzi ambapo vitisho na kunyimwa taarifa wanazozihitaji jambo ambalo hupelekea ugumu katika kutekeleza kazi za kihabari.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanalenga kuwanoa waandishi wa habari 25 (Unguja 15 na Pemba 10) kwa ikiwa ni kuwaongezea ujuzi katika uandishi wa habari za mapitio ya sheria za habari na uhuru wa habari visiwani Zanzibar.