Katika juhudi za kuimarisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na kukuza haki za kidemokrasia, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA- ZNZ) kimetoa mafunzo ya siku mbili kwa Wahamasishaji Jamii (Citizen Brigades) wapatao 60 kwa upande Unguja ambapo ni sehemu ya programu ya kuimarisha uongozi kwa wanawake (SWIL) wenye lengo la kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia kwa kuwawezesha wanawake kushika nafasi katika ngazi za maamuzi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano TAMWA ZNZ, Saphia Ngalapi, ameeleza kuwa watekelezaji wa programu wana imani na wahamasishaji waliopatiwa mafunzo na kuwa watakuwa mabingwa wa kuhamasisha jamii juu ya haki za wanawake kushiriki katika uongozi.
“Kupitia timu hii, tunatarajia mabadiliko kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki ya demokrasia na maendeleo kwa mwanamke kufikia 50% kwa 50% katika ngazi za maamuzi,” alisema Ngalapi.
Afisa Ufuatiliaji na Tathmini TAMWA ZNZ, Mohamed Khatib, aliwasisitizia wahamasishaji hao juu ya umuhimu wa kazi yao katika kukuza nafasi za wanawake katika uongozi.
“Uchaguzi wa 2025, tunataka tuone wanawake wanashika nafasi za uongozi kuanzia ngazi za shina hadi Taifa, na tufahamu kuwa hii si ajira bali ni kazi ya kujitolea kuhakikisha matarajio ya wanawake kushika nafasi za uongozi yanafikiwa kwa kubadilisha mitazamo ya jamii,” alifafanua afisa huyo.
Mafunzo haya yamejumuisha wawakilishi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo viongozi wa dini, watu wenye ulemavu, wanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji na wanaume wa mabadiliko.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya TAMWA ZNZ, Asha Abdi ambae ni mkufunzi katika mafunzo hayo ya siku mbili, aliwahimiza wahamasishaji jamii kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha malengo ya mradi huu yanafikiwa.
Ukhty Amina Salum ambae ni kiongozi wa dini na mwanaharakati wa siku nyingi ameeleza shukrani zake kwa kuchaguliwa kuwa sehemu ya wahamasishaji wa jamii. “Nafurahi kuwa miongoni mwa wahamasishaji wa jamii, dhamana hii nitaibeba na kuhakikisha jamii inahamasika na kuachana na dhana potofu juu ya uwezo wa mwanamke na maamrisho ya dini kuhusiana na wanawake kushiriki katika uongozi. alisema Ukhty Amina.
Nae Haji Khamis Haji kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja alisisitiza kuwa elimu aliyoipata itamsaidia kuhamasisha jamii katika mkoa wake kutambua haki zao za kidemokrasia na kuongeza wanawake katika nafasi za uongozi.
Mafunzo haya yanaashiria jitihada za pamoja kati ya TAMWA- ZNZ na washirika wake katika kuwaandaa wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kuelekea uchaguzi wa 2025, huku wakilenga kuongeza idadi ya wanawake katika ngazi za maamuzi visiwani Zanzibar.