
CADiR kuwezesha Elimu, Afya na Uchumi kwa Watu Wenye Ulemavu.
Kuzinduliwa kwa program mpya ya kukuza na kuimarisha haki, fursa na ustawi wa watu wenye ulemavu (CADiR) Tanzania kutasaidia watu wenye ulemavu kufikiwa na kupata fursa sawa na watu wengine bila ya kubaguliwa.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman alipokuwa akizindua program hiyo katika hotel ya Madinatul-Bahar, Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar na kusisitiza kuwanprogramu hiyo itasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu, hasa ikizingatiwa kwamba idadi yao imekuwa ikiongezeka kwa kasi kubwa.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, idadi ya watu wenye ulemavu imeongezeka kutoka asilimia 5.8 mwaka 2012 hadi asilimia 11.4 mwaka 2022. Mheshimiwa Othman alisema takwimu hizi zinadhihirisha haja ya kuimarisha huduma, fursa na mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu ili wasiachwe nyuma katika maendeleo ya taifa.
Alieleza kuwa Serikali tayari imeweka mikakati kadhaa, ikiwemo kutungwa kwa Sera ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2018 na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 8 ya mwaka 2022. Hatua nyingine ni kuanzishwa kwa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu na mabaraza yake ya wilaya, pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu.
Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mpango wake wa mwaka 2025–2030 imedhamiria kuongeza ushiriki wa watu wenye ulemavu katika ngazi za maamuzi kutoka asilimia 2 hadi asilimia 5. Pia, imepanga kuimarisha mifumo ya utambuzi wa awali wa ulemavu na kuendeleza miundombinu rafiki ikiwemo shule, hospitali na barabara ili kurahisisha maisha yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi wa NAD-Zanzibar, Ndugu Abdalla Amour, alisema CADiR inalenga kugusa maeneo muhimu ya maisha ya watu wenye ulemavu. “Programu hii inatoa kipaumbele katika elimu mjumuisho, uwezeshaji kiuchumi, afya na marekebisho, pamoja na uhamasishaji na utetezi wa haki za watu wenye ulemavu,” alisema.
Ameongezea kuwa, program hiyo ya miaka mitano (2025- 2029) inatarajiwa kutekelezwa katika wilaya zote 11 za Zanzibar na katika mikoa tisa ya Tanzania Bara, ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Kigoma, Dodoma, Manyara, Kagera na Singida na kushirikisha mashirika mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwemo TAMWA-ZNZ, SHIJUWAZA, ZANAB, CHAVITA, MADRASA, SHIVYAWATA na Mnazi Mmoja Hospital.