
21/09/2025
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
JAMII YASHAURIWA KUACHA KUWACHUKUA WATOTO KWENYE
MIKUTANO YA KAMPENI ZA UCHAGUZI
Jamii imeshauriwa kuacha tabia ya kuwachukua watoto kwenye mikutano ya kampeni
zinazoendelea kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Indhari hiyo imetolewa na Taasisi zinazojihusisha na masuala ya wanawake na uongozi
Zanzibar zikiwasisitiza wazazi na walezi kuwa hatua ya kuwahusisha watoto kwenye
mikutano hiyo inawaweka katika mazingira yasiyo salama na kuwanyima haki ya malezi
bora, huku wakishuhudia matendo na mienendo isiyofaa kwa umri wao.
Taasisi hizo ikiwemo Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA),
Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO), Jumuiya ya Wanasheria
Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania,
Zanzibar (TAMWA-ZNZ) zimesema watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wanapaswa
kulindwa na kupewa nafasi ya kukua katika mazingira salama na yenye staha,
kuwahusisha katika mikutano ya kisiasa, ambayo mara nyingi huambatana na
msongamano na kelele, kunahatarisha afya na usalama wao.
Zimesema mbali na athari za kimwili, watoto huathirika kisaikolojia kutokana na
kushuhudia mambo yasiyofaa kwa umri wao, kwa kuwa watoto sio wapiga kura, uwepo
wao kwenye mikutano hiyo hauna tija yoyote na badala yake unawaweka kwenye
mazingira yasio sahihi kwao.Pia zinaikumbusha jamii kwamba usalama na afya ya mtoto ni jukumu la pamoja, na kila
mmoja ana wajibu wa kuhakikisha watoto wanabaki katika mazingira salama kama
nyumbani, madrasa na skuli.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Zanzibar Na. 6 ya mwaka 2011 inaeleza wazi juu ya
ulinzi wa watoto, Kifungu cha 14(1) Mtoto anatakiwa kulindwa dhidi ya mazingira
yanayoweza kuhatarisha maisha au afya yake.
Tanzania ikiwemo Zanzibar imeridhia mikataba mbali mbali ya ulinzi wa mtoto ikiwa ni
pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto (CRC) wa 1989, kupitia Kifungu cha
19 na 32, vinasisitiza ulinzi wa mtoto ili kujenga jamii yenye heshima na ustawi, na
Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa 1990, katika Kifungu cha
15 na 16, kinacholinda mtoto dhidi ya mazingira yoyote hatarishi kiafya na kijamii.
Taarifa hiyo imesema hivi karibuni kumejitokeza tabia ya kuwachukua ama kuwaacha
watoto kuzurura katika maeneo yanayofanyiwa kampeni na hivyo kuwa katika hatari ya
kuweza kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji ama ukatili wa aina yeyote.
Kutowapeleka watoto katika mikutano ya kampeni kutawakinga watoto kukumbana na
vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa aina mbali mbali ambapo kwa mujibu wa Takwimu
za Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar (OCGS), matukio ya ukatili na
udhalilishaji dhidi ya watoto yamekuwa yakiongezeka kila mwezi.
Takwimu hizo zinaonesha ongezeko la matukio hayo ambapo mwezi Juni 2025
yaliripotiwa matukio 97 huku waathirika watoto wakiwa 83 sawa na asilimia 85.6 ya
matukio yote, mwezi wa Julai 2025, jumla ya matukio 107 yaliripotiwa huku waathirika
wengi wakiwa watoto ambao ni 95 sawa na asilimia 88.8 na kwa upande wa mwezi wa
Agosti 2025 matukio yalikuwa 116, matukio yaliyohusisha watoto ni 104 ambapo ni sawa
na asilimia 89.7.
Taasisi hizo zinatoa wito kwa wazazi, walezi, viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na
vyombo vya habari kushirikiana kwa karibu katika kutoa elimu na kuchukua hatua za
kuwalinda watoto.JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway
zimeungana kuhamasisha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi katika nyanja
mbali mbali.
Imetolewa na
JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA Zanzibar.