Edit Content

About Us

TAMWA is a national level Non-Governmental Organization known as Tanzania Media Women’s Association formed in 1987. TAMWA Zanzibar became fully self-governing and operational in both Isles of Unguja and Pemba since 2004. In January 2007, it attained its own separate registration.

Contact Info

Taarifa ya Tafakari na Kukabidhi Uongozi

Taarifa ya Tafakari na Kukabidhi Uongozi
Safari Yangu na TAMWA–Zanzibar
Ndugu Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya TAMWA, ZNZ
Wajumbe wa Bodi,
Wanachama wa TAMWA, ZNZ
Uongozi wa utendaji wa TAMWA, ZNZ
Ndugu wageni waalikwa
Ndugu waandishi wa Habari,
Assalamu aleykum,
Kama kuna kundi moja la watu wanaojua kuuliza maswali magumu, kufuatilia ukweli bila
kuchoka, na bado malipo yakawa madogo ama hakuna kabisa, basi hao ni waandishi wa
habari. Cha kufurahisha zaidi ni kwamba, hao hao ndio nguzo kuu ya TAMWA–Zanzibar.
Ndugu waandishi wa Habari, nashukuru sana kwa kuitikia wito wetu huu kufika hapa
kujumuika na sisi na mimi hasa kipekee kwa kuuaga umma Wazanzibari na Tanzania kwa
jumla kama Mkurugenzi wa TAMWA, ZNZ katika miaka yangu yote nilyoifanyia kazi taasisi.
Asaanteni sana.
Ushiriki wangu wa moja kwa moja na TAMWA Zanzibar ulianza rasmi mwaka 2002, kipindi
ambacho TAMWA ilikuwa ni 1 tu na ilipata mradi wa mwaka mmoja wa Ukatili dhidi ya
Wanawake na Watoto na ambao ulitekelezwa na Mratibu dada Shifaa Said.
Hivyo, Mratibu wa mradi ule alifanya kazi kubwa sana na kutushirikisha vijana wengi
nikiwemo na mimi na niliweza kujifunza zaidi masuala ya wanawake na watoto.
Nakumbuka nilivyokuwa nikihoji sana masuala ya haki za wanwake na watoto kwa chombo
changu cha Habari, Wakati ule Gazeti la Nuru. Nilibahatika kujiunga na TAMWA mwaka
2003 na pia kuingia katika bodi ya utendaji. Kiasi ambacho mradi ulipomalizika TAMWA
ikasema ifunge Afisi zake Zanzibar zilizokuwepo pale Weles, nikaweza kusema imara
kwenye bodi pamoja na mwenzangu bi Nassra Mohammed kusema hapana kwa vile mradi
ulishafanya mengi na tunahitaji kuyaendeleza na siyo kurudi nyuma. Ilikuwa ni ngumu
kuishawishi bodi, kwa vile hakukuwa na rasilimali za kushughulikia lakini kwa busara ya
bodi yetu ya TAMWA na sisi kuahidi kuisimamia katika hali hiyo hivyo tulifanikiwa kuiweka.
Niwashukuru sana hapa Mkurugenzi aliyekuwepo bara wakati ule, Dkt. Ananilea Nkya na
Dada Shifaa Said na Bi Nassra Mohammed na wajumbe wote wa bodi kwa kuwa pamoja
katika hili. Kipekee watu hawa walikuwa ni zaidi ya colleagues walikuwa ni walimu na
walezi wangu.Afisi iliendelea haidhuru ilikuwa kwa shida mana binafsi nilipata uhamisho wa kikazi
kwenda Afisi ya Raisi na pia nilikwenda kufanya masomo yangu ya shahada ya pili kuanzia
mwaka 2004 hadi 2006. Hata hivyo, mwaka 2006 ilibidi kutafuta usajili wa TAMWA, ZNZ
kwa vile sheria ya NGO kule bara ilibadilika mwaka 2002 na kukataza mashirika kufanya
kazi kote kwa usajili mmoja. Nashukuru mimi na mwenzangu bi Nassra tulihangaika
kutafuta usajili nenda rudi kwa mwaka ule na kwa bahati pia katika mambo kadhaa ya
kufatilia wakaja wenzetu wa Care tuandae mradi pamoja. Hilo nalo lilikuwa ni tatizo
jengine wakati sikuwa na uzoefu wa kuandika miradi wala kutekeleza na kutokujua kabisa
lugha hiyo Care wao wakawa na mtaalamu kutoka Afrika ya kusini na sisi TAMWA
mtaalamu ni mimi nisiyejuwa chochote. Nililazimika kujifunza na kwenda kwenye
mitandao wakati ule ukilipia shilingi 500, nilisoma kama mtoto wa skuli ili nisije kuadhirika
pamoja na taasisi yetu.
Nashukuru kusema mwaka 2007 ukawa ni wa manufaa zaidi mana tulipata usajili wetu
mapema Januari na pia majibu ya mradi tuliondika na Care yakawa mazuri hivyo tukapata
mradi wa Women Empowerment in Zanzibar (WEZA) mwaka 2008 hadi 2011.
Tukautekeleza kwa ujasiri mkubwa na kipekee hapa naomba niwatambue wajumbe
wenzangu tulioanza awamu hii mpya pamoja akiwemo dada Asha Abdi, dada Halima
Msellem, dada Mwanakhamis Mrisho na dada Jitihada Abdalla. Kwa kweli walijitoa na
walifanya kazi kwa mapenzi makubwa ya kuleta mabadiliko ya wanawake na watoto
nchini ilikuwa kiuchumi lakini ikenda hata kiuongozi na kijamii na pia tukaanza kutafuta
kiwanja na ujenzi wa jengo letu hili la Tunguu. Asanteni sana. Mwaka huu pia ndipo
nilipoanza kufanya kazi na TAMWA, ZNZ rasmi na hivyo kuchukua likizo bila malipo kutoka
kwa mwajiri wangu Serikalini.
Na ni mwaka huu wa 2008 ndipo pia safari yangu ya huba na nyinyi ndugu waandishi wa
Habari ilipoanza. Tulianza safari ndefu ya kujenga taasisi imara katika jamii ambako
mfumo dume haukuwepo tu katika mila, bali pia katika mifumo, sheria, na taratibu rasmi.
Haikuwa safari nyepesi. Kulikuwepo changamoto, upinzani, uhaba wa rasilimali, na
nyakati za kutoeleweka. Lakini kama ilivyo kwa uandishi wa habari wenyewe,
changamoto hizo ndizo zilijenga uthabiti wetu kupitia kufichua mila potofu kama dago
ambapo wanaume huwenda kuvua na kuwaacha wanawake na watoto
kutokuwashughulikia. Alitupigia simu Afisa mmoja wa elimu kusema tunataka kuharibu
mwenendo mzuri wa maisha ya watu kwa kuwatia fitna wake zao mana hilo ilikuwa ni
jambo la kawaida kwao wameishi nalo kwa miaka mingi. Kesi za ukatili wa kijinsia (GBV)
na wakati mwengine migongano na wenzetu wa polisi na kubwa pia lilikuwa la Mahakama
ya Kadhi.Leo, TAMWA–Zanzibar inasimama kama taasisi yenye nguvu, heshima, na uaminifu
mkubwa, ikiwa na:
Wanachama 82 waandishi wa habari kutoka Unguja na Pemba;
Wafanyakazi 23 waliobobea, wenye kujituma na weledi wa hali ya juu;
Mifumo thabiti ya kifedha inayosimamiwa na wahasibu wenye ithibati ya CPA;
Ripoti za kila mwaka za kifedha, kiprogramu na kitaasisi zinazowekwa wazi kwenye
mitandao;
Ukaguzi wa hesabu unaofanywa na kampuni iliyosajiliwa na Bodi ya Taifa ya
Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu.
Haya yote hayakutokea kwa bahati. Yalitokana na mshikamano, uvumilivu, na imani ya
pamoja kwamba haki ya kijinsia si ombi bali ni haki ya msingi.
Tulichokifanya Pamoja
Kwa kushirikiana na waandishi wa habari, jamii, washirika wa maendeleo, na taasisi
mbalimbali:


Tuliwafikia wanawake na watu wenye ulemavu zaidi ya 11,120 kupitia vikundi
572 vya kuweka na kukopa, tukibadili mazingira ya utegemezi kuwa ya uongozi
na kujitegemea;
Tulipambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Kutoka
katika mazingira ya awali yasiyo na sheria bora, kutokuwa na kesi za vifungo,
hadi kufikia kupata sheria nzuri na hivyo kutoa adhabu kwa washitakiwa. Sheria
hizo ni pamoja na Marekebisho haya ya kisheria yalijumuisha Sheria ya
Ushahidi Na. 9 ya mwaka 2016, inayoruhusu matumizi ya ushahidi wa
mazingira (circumstantial evidence) na ushahidi wa shahidi mmoja pekee,
ikiwemo mtoto, katika kesi za ukatili wa kijinsia; Sheria ya Mahakama ya Kadhi
Na. 9 ya mwaka 2017, ambayo inatambua mgawanyo wa mali za ndoa pale
ndoa inapovunjika; na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Na. 7 ya
mwaka 2018, inayoruhusu. Tumeshuhudia sasa adhabu na mifumo ya GBV
ikiwemo kuripotiwa kesi na Afisi ya Mtakwimu Mkuu ambapo wanaopata
adhabu ama vifungo wamekuwa wakiongezeka hadi mwaka 2024 kulikuwa na
asilimia 16 ya vifungo kutoka kwa kesi 1,809 kulingana na Ripoti ya Mtakwimu
Mkuu wa Serikali ya mwaka 2025. Tunashukuru pia kwa tuzo mbalimbali
tulizopokea, ikiwemo kutambuliwa kama mmoja wa watumiaji bora wa
takwimu za kitaifa;




Tulichangia ongezeko la uwakilishi wa wanawake katika siasa na nafasi za
maamuzi, ambapo sasa tunakaribia asilimia 35 ya wanawake katika ngazi za
maamuzi kuanzia taifa hadi masheha, sambamba na kukuza ushindani wa
kidemokrasia.
Tulianzisha na kuimarisha mifumo ya Tahadhari ya Mapema dhidi ya Ukatili wa
Kisiasa
kwa Wanawake, kwa kushirikiana na AZAKI 47.
Tulishiriki kikamilifu katika mapitio na marekebisho ya sera na sheria kandamizi,
na kutetea uhuru wa vyombo vya habari pamoja na haki ya kupata taarifa.
Kupitia mradi wa ZanzAdapt, tulibadilisha simulizi la mabadiliko ya tabianchi na
kuimarisha uandishi unaozingatia jinsia, tukizalisha hadithi 116 ndani ya mwaka
mmoja.
Na kwa fahari kubwa, tumepata majengo yetu wenyewe yanayotuhifadhi kama
taasisi na pia yameanza kuingiza kipato kupitia upangishaji.
Shukrani za Dhati
Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa:
 Bodi ya Wakurugenzi wa TAMWA–ZNZ kwa uongozi, ushauri na imani yao, bodi
hii pamoja na zote zilizopita; Bodi ya Zanzibar na pamoja na ya TAMWA bara
kwa usimamizi, kunipa mielekeo na maono mbali mbali.
 Wanawake na wanaume wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, ambao ndio
walengwa na nguzo ya kazi yetu;
 Asasi za kiraia (CSOs) tulizoshirikiana nazo katika ngazi zote;
 Taasisi za Serikali, hasa Wizara ya Jinsia, Wizara ya Habari, Afisi ya Msajili wa
NGOs na Afisi ya Mtakwimu Mkuu kwa ushirikiano, majadiliano, na hata
changamoto zilizotujenga;
 Washirika wa maendeleo na wafadhili, kwa kuamini dira na kazi ya TAMWA–
ZNZ; hasa Ubalozi wa Denmark, Ubalozi wa Norway, UNFPA na UNWOMEN.
 Zaidi sana, waandishi wa habari, moyo, sauti, na dira ya taasisi hii
 Maalumu niwashukuru wafanyakazi wote wa TAMWA, ZNZ ambao kati yao
walikuwa ni wajumbe wa TAMWA. Haikuwa kazi rahisi kuijenga TAMWA, ZNZ
kuna wakati najua wengine mlipitia maumivu makubwa na kufanya kazi katikati
ya changamoto zenu wenyewe na kwa jumla naambiwa si mtu rahisi
kufanya kazi nami. Mlinivumilia nashukuru sana kwa upendo wenu kwangu.
Kuna wengine tumefanyakazi zaidi ya miaka 10 akiwemo dada Asha Abdi,
Mohammed Ali (dereva), mtu wa Utawala dada Zamoyoni Vuai, Mhasibu Mkuu
dada Khalda n.k Naushukuru pia uongozi wa TAMWA, ZNZ. Akiwemo Programu
Manager mwenyewe sasa Mkurugenzi dada Nairat, Mkuu wa Fedha na Utawala,
HOFA, Mtaalamu wa M&E Mohammed Khatibu, dada Sophia Ngalapi mkuu wa
mawasiliano, dada Fathiya Mussa aliyekuwa Mratibu wa Pemba na dada Tatu
Mtumwa. Asanteni sana.
Shukrani za pekee ziende kwa familia yangu watoto wangu na mume wangu
kwa uvumilivu pia mkubwa, hasa katika vipindi vigumu ambavyo taasisi
haikuwa na hata fedha ya mshahara wangu mdogo, ikiwemo mwaka mzima
wa 2012 na 2013 baada ya kumaliza mradi wetu wa WEZA ambapo hatukuwa
na wafanyakazi tena si kwa Care wala TAMWA, huku Mfadhili (Umoja wa Ulaya)
akidai ripoti zake za mwisho, za miaka minne, za miaka miwili, za mwaka
mmoja na miezi sita na wakati huo huo mkataba wangu wa kufanyakazi bila
ya malipo kutoka Serikalini umemalizika. Hivyo nililetewa barua ya mwisho
kuamua nirudi kwa muajiri wangu Serikali ama niache kazi. Nashukuru
kutokana na mashirikiano na wadau nyote pamoja na familia kunipa baraka
nikaweza kuchagua la pili ili niweze kuendeleza gurudumu hili la kuleta
mabadiliko chanya kwa wanawake, Watoto na jamii kwa jumla. Nawashukuru
nyote pamoja hasa na dada Mwanakhamis Mrisho na familia kwa kunishika
mkono huku.
Kukabidhi Uongozi
Kwa heshima na uwazi, napenda kuutaarifu umma kwamba nimekabidhi rasmi majukumu
yangu kama Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ. Uongozi sasa uko mikononi mwa Bi. Nairat
Abdulla, kiongozi mwenye uwezo, maadili, na maono yanayoendana kikamilifu na
dhamira ya TAMWA-ZNZ. Wengi wenu mnamfahamu hasa kwa msimamo wake, nidhamu
ya muda (deadlines), na uzingatiaji wa taratibu na sheria za taasisi. Nina imani kubwa
kwamba ana uwezo wa kuipeleka TAMWA-ZNZ mbali zaidi.
Nawaomba kwa dhati waandishi wa habari, wanachama, wadau, na umma kwa ujumla
kumpa Bi. Nairat ushirikiano mkubwa kama mlivyonipa mimi, na hata zaidi ili TAMWA-
Zanzibar iendelee kupaa, kukua, na kutimiza malengo yake kwa kiwango cha juu zaidi.
Taasisi imara haijengwi na mtu mmoja. Huimarika pale uongozi unapobadilika, lakini dira
ikibaki ile ile.
Hitimisho
Siondoki kwenye harakati.
Siondoki kwenye mapambano ya haki na usawa.
Ninabadilisha nafasi ili taasisi iendelee kuishi, kukua, na kung’ara.Kama mwandishi mzuri wa habari anavyojua:
hadithi haimaliziki hubadilisha tu msisitizo (angle of the
story).
Asanteni sana.
Mkurugenzi aliyemaliza muda wake TAMWA, ZNZ
Dkt. Mzuri Issa Ali

Subscribe to our
News and Presses

***We Promise, no spam!

A national level Non-Governmental Organization known as Tanzania Media Women’s Association formed in 1987.The registration number is 493 under Zanzibar Society Act No. 6 of 1995

We’re Available

Monday : 08.00 - 10.00
Tuesday : 08.00 - 10.00
Wednesday : 08.00 - 10.00
Thursday : 08.00 - 10.00
Friday : 09.00 - 07.00
Saturday : 10.00 - 05.00
Sunday : 10.00 - 05.00