Wanachama 20 wa Kijaluba iSAVE Wanufaika na Mafunzo ya Batiki na Ushonaji
“Waiahidi TAMWA-ZNZ kuyaendeleza kivitendo mafunzo hayo”

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), kwa kushirikiana na wadau wa Mradi wa CADiR kupitia programu ya EEP, kimeendesha mafunzo ya vitendo ya utengenezaji wa batiki na ushonaji kwa wanachama 20 wa vikundi vya Kijaluba iSAVE kutoka vikundi saba (7) vinavyotekeleza shughuli zao katika wilaya tatu za Unguja.
Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha washiriki kupata ujuzi wa amali utakaowasaidia kuanzisha na kuimarisha shughuli za uzalishaji mali (Income Generating Activities – IGAs), kuongeza kipato cha kaya na kujenga ustahimilivu wa kiuchumi kwao na familia zao.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Afisa Programu wa Uwezeshaji Kiuchumi (EEP) ambaye pia ni Afisa Mkuu wa Programu wa TAMWA-ZNZ, Zaina Mzee alisema uwekezaji katika ujuzi wa vitendo ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha watu wenye ulemavu, wanawake na walezi wa watoto wenye ulemavu kiuchumi.

“Ujuzi wa vitendo kama batiki na ushonaji ni njia ya moja kwa moja ya kuwawezesha wanawake kujenga uwezo wa kujitegemea kiuchumi. Tunataka kuona wanachama wa Kijaluba iSAVE wakitumia ujuzi huu kuanzisha na kukuza biashara endelevu zinazoboresha maisha yao,” alisema Zaina Mzee.
Washiriki walipata mafunzo ya vitendo kuhusu mbinu za utengenezaji wa bidhaa za batiki, ushonaji, ubora wa bidhaa, pamoja na mikakati ya kuzalisha bidhaa zinazoweza kushindana katika soko. Ujuzi huo unatarajiwa kuwa chachu ya kuwawezesha kuanzisha au kupanua biashara zao na kuongeza thamani ya shughuli zao za kiuchumi.
Mmoja wa washiriki Aisha Juma Ibrahim alieleza kufurahishwa na mafunzo hayo, akisema:

“Mafunzo haya yametufungua macho. Sasa tuna ujuzi ambao tunaweza kuutumia kuanza uzalishaji na kuongeza kipato cha familia zetu. Tunashukuru TAMWA-ZNZ na wadau kwa kutuwezesha,” alisema mshiriki huyo.
Katika hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo, wahitimu walikabidhiwa vyeti vya ushiriki kama ishara ya kutambua mafanikio yao na hatua waliyofikia katika kujenga uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Mafunzo ya batiki na ushonaji ni sehemu ya afua za Uwezeshaji Kiuchumi (EEP) zinazotekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na SHIJUWAZA, NAD-ZNZ na ZANAB chini ya Programu ya CADiR ambapo mafunzo hayo yataendelea kuwafikia wanachama wengine wa vikundi vya Kijaluba iSAVE kwa Unguja na Pemba kupitia fani mbalimbali zikiwemo utengenezaji wa unga wa lishe, ufugaji wa kuku, kilimo cha mbogamboga na ushonaji, kwa lengo la kuimarisha uwezo wao wa kujitegemea kiuchumi na kuboresha maisha yao.
