Elimu Yaiwezesha Jamii Kutambua na Kuripoti Udhalilishaji Zanzibar

Mabadiliko chanya katika kuzuia na kupambana na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto yameanza kuonekana katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, huku jamii ikionyesha kuongezeka kwa uelewa wa kutambua vitendo vya ukatili, kutoa taarifa na kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo.

Mabadiliko hayo yamebainika katika Mkutano wa Tathmini wa Mradi wa “Tunaweza Pamoja”, unaotekelezwa na TAMWA Zanzibar kwa ufadhili wa UN Women kupitia mradi wa Kukomesha Ukatili Dhidi ya Wanawake na Wasichana (EVAWG).

Mkutano huo uliofanyika Gamba, Wilaya ya Kaskazini A, uliwakutanisha wadau 29 kutoka wilaya mbalimbali za Zanzibar, wakiwemo viongozi wa dini, Masheha, Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals), wanachama wa GBV Network, Mamalishe, Waratibu na waendesha bodaboda.Wadau hao walitathmini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza pamoja na hatua zinazohitajika ili kuendeleza mapambano dhidi ya udhalilishaji.

Watoto waanza kutambua udhalilishaji

Katika Shehia ya Fukuchani, Wilaya ya Kaskazini A, Sheha wa eneo hilo, Haji Mohamed Juma, alisema elimu iliyotolewa imeanza kuwajengea watoto uwezo wa kutambua vitendo vya udhalilishaji na kutoa taarifa.

Alisema, baadhi ya watoto wenye umri wa miaka sita, saba na minane tayari wameanza kuelewa viashiria vya udhalilishaji na kuwa na ujasiri wa kutoa taarifa wanapobaini vitendo visivyofaa.

“Watoto wawili walinifuata na kunipa taarifa kuhusu mtoto mwenzao kwamba anafanya vitendo vibaya kwa mtoto mwenzake. Nilifuatilia na kubaini kuwa ni kweli. Hii inaonyesha kuwa watoto wana uelewa wa kutambua udhalilishaji na viashiria vyake,” alisema Haji.

Alisema, elimu hiyo inapaswa kuanza kutolewa tangu ngazi ya chekechea ili kuwajengea watoto msingi wa kujilinda na kutambua mazingira yasiyo salama.

Wasichana mahotelini wajengewa uelewa

Mabadiliko mengine yameonekana miongoni mwa wasichana wanaofanya kazi katika sekta ya hoteli.

Asia Fadhil Makame msaidizi wa Sheria wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, alisema elimu aliyopata kupitia TAMWA Zanzibar imemsaidia kuwafikia wasichana wanaofanya kazi katika hoteli na kuwaelimisha kuhusu haki zao na namna ya kuripoti udhalilishaji.

Alisema, baadhi ya wasichana wamekuwa wakikabiliwa na vitisho vya kufutwa kazi kwa sababu hawana mikataba, huku wengine wakishinikizwa kutoa rushwa ya ngono ili waendelee na ajira.

“Tumeweza kutembelea mahotelini na kugundua wasichana wengi wanafanyiwa vitisho vya kufutishwa kazi kwa sababu hawana mikataba. Wengine huombwa rushwa ya ngono ili waendelee na kazi,” alisema Asia.

Aidha alisema kuwa , elimu hiyo imewasaidia baadhi ya wasichana kutambua kuwa vitendo hivyo ni udhalilishaji, kujua namna ya kuripoti na kuchukua hatua dhidi ya mazingira yasiyo salama kazini.

Wanawake wavuvi wapata mazingira salama

Katika Shehia ya Kinduni, Wilaya ya Kaskazini B, mabadiliko yameonekana pia miongoni mwa wanawake wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi.

Mratibu wa Shehia hiyo, Bahati Juma Chumu, alisema elimu iliyotolewa imewasaidia wanawake hao kuchukua tahadhari zaidi wanapoingia baharini.

Alisema kuwa ,wanawake hao walishauriwa kutumia vipolo wanapoingia baharini ili kujisitiri na kupunguza uwezekano wa miili yao kuonekana kutokana na nguo kulowa.

“Mara nyingi maeneo ya bandarini, kina mama wanapoingia baharini kufuata samaki, nguo zao hulowa sana na kupelekea maumbile ya miili yao kuonekana, hivyo ni rahisi kudhalilishwa aidha kwa maneno au vitendo,” alisema Bahati.

Alisema ushauri huo umepokelewa na wanawake hao na umechangia kuwafanya wajisikie salama na huru zaidi wanapofanya shughuli zao.

Uelewa waongezeka kwa Mamalishe

Katika maeneo ya masoko, Yumna Nassor Ali, ambaye ni Mamalishe, alisema elimu kuhusu udhalilishaji imeleta mabadiliko katika mtazamo wa jamii kuhusu wanawake wanaofanya biashara ya chakula.

Alisema dhana kwamba Mamalishe wanahusishwa na biashara ya miili imekuwa ikichangia unyanyapaa dhidi yao, lakini elimu imeanza kubadili mitazamo hiyo.

“Imezoeleka kwamba Mamalishe wanauza chakula na kuuza miili yao, lakini sasa hivi maeneo mengi ya masokoni uelewa kuhusu masuala ya udhalilishaji umekuwa mkubwa sana,” alisema Yumna.

Alisema, kuongezeka kwa uelewa kumewasaidia wanawake hao kujitambua, kujiheshimu na kuelewa haki zao wanapokabiliwa na vitendo vya udhalilishaji.

Watoto Nungwi waanza kutoa taarifa

Huko Shehia ya Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Nachumu Rashid Haji alisema watoto wameanza kuwa na uelewa wa kutambua mazingira ambayo yanaweza kuwaweka katika hatari.

Alitoa mfano wa tukio ambapo baadhi ya watoto walipewa zawadi na mtu kutoka jamii ya Kimasai, huku mmoja wao akiondoka naye.

Nachumu alisema watoto hao walitoa taarifa kuhusu tukio hilo, jambo alilolieleza kuwa ni ishara ya kuongezeka kwa uelewa wao kuhusu usalama na mazingira yasiyofaa.

“Watoto wa skuli walikuja kunifuata na kusema kwamba wamepewa zawadi na Mmasai, lakini mmoja kati yao aliondoka na Mmasai huyo,” alisema Nachumu.

Alisema tukio hilo lilifuatiliwa na kutoa umuhimu wa jamii kuwa macho na kuhakikisha watoto wanafundishwa namna ya kutambua mazingira hatarishi na kutoa taarifa mapema.

Viongozi wa dini muhimu katika mapambano

Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa wadau, Lucy Tesha, Mtaalamu wa Programu wa EVAWG kutoka UN Women, alisema viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kuelimisha jamii kutokana na ushawishi wao katika masuala ya mienendo na maadili.

“Ninaamini viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa katika jamii, hasa katika masuala ya mienendo na tamaduni, na hivyo ni rahisi kuweza kushughulikia masuala ya udhalilishaji katika jamii katika ngazi zote,” alisema Lucy.

Alisema ushirikishwaji wa viongozi wa dini pamoja na makundi mengine ya jamii unaweza kusaidia kufikisha ujumbe wa kupinga udhalilishaji kwa watu wengi zaidi.

TAMWA Zanzibar: Watoto kutoa taarifa ni mafanikio

Kwa upande wake, Mohamed Khatib Mohammed, Afisa wa Ufuatiliaji na Tathmini TAMWA Zanzibar, alisema uwezo wa watoto wadogo kutambua na kuripoti vitendo vya ukatili ni miongoni mwa matokeo muhimu ya mradi.

“Matokeo haya ni muhimu sana kwetu, hasa kuona watoto wenye umri wa miaka sita na saba sasa wanaweza kuelewa ukatili na udhalilishaji wa kijinsia na hata kuripoti matukio hayo kwa walezi wao,” alisema Mohamed.

Alisema mafanikio hayo yanaonyesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii, hususan watoto, wazazi, viongozi wa jamii na makundi mengine yenye ushawishi.

Hatua zaidi zahitajika

Mkutano huo ulisisitiza umuhimu wa kuendeleza elimu na uhamasishaji katika jamii ili kuhakikisha mabadiliko yaliyopatikana yanaendelea kuwa endelevu.

Wadau walieleza kuwa pamoja na hatua zilizopigwa, bado kuna umuhimu wa kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa, kuongeza uelewa wa haki, kuwajengea uwezo watoto na wanawake, pamoja na kuhakikisha waathirika wa udhalilishaji wanapata msaada na ulinzi unaohitajika.

Kwa ujumla, uzoefu kutoka Fukuchani, Kinduni, Nungwi na maeneo mengine unaonyesha kuwa elimu ya jamii inaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuzuia udhalilishaji.

Kuanzia watoto wanaojifunza kutoa taarifa, wanawake wanaojua haki zao kazini, hadi viongozi wa jamii wanaochukua hatua, mabadiliko hayo yanaonyesha kuwa mapambano dhidi ya udhalilishaji yanahitaji ushiriki wa jamii nzima na kuendelea kwa elimu katika ngazi zote.

Mkutano huo uliofanyika Gamba, Wilaya ya Kaskazini A, uliwakutanisha wadau 29 kutoka wilaya mbalimbali za Zanzibar, wakiwemo viongozi wa dini, Masheha, Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals), wanachama wa GBV Network, Mamalishe, Waratibu na waendesha bodaboda.Wadau hao walitathmini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza pamoja na hatua zinazohitajika ili kuendeleza mapambano dhidi ya udhalilishaji.

Subscribe to our
News and Presses

***We Promise, no spam!

A national level Non-Governmental Organization known as Tanzania Media Women’s Association formed in 1987.The registration number is 493 under Zanzibar Society Act No. 6 of 1995

We’re Available

Monday : 08.00 - 10.00
Tuesday : 08.00 - 10.00
Wednesday : 08.00 - 10.00
Thursday : 08.00 - 10.00
Friday : 09.00 - 07.00
Saturday : 10.00 - 05.00
Sunday : 10.00 - 05.00