Zanzibar, 22 Novemba 2026
TAMWA-ZNZ kupitia Programu ya CADiR imeendesha mafunzo ya siku tatu kwa wanachama wa vikundi 22 vya KIJALUBA iSave kutoka Wilaya ya Kati, Kusini na Kaskazini ‘B’ Unguja, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutafuta masoko, kutangaza bidhaa na kutumia vifungashio bora vinavyoongeza thamani na ushindani wa bidhaa zao.
Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wanavikundi, wakiwemo watu wenye ulemavu, kuboresha shughuli zao za uzalishaji na biashara kwa kuwapatia maarifa ya vitendo kuhusu namna ya kuandaa bidhaa, kuzifungasha kwa ubora na kuzitangaza ili kuvutia wateja na kuongeza mauzo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Programu wa Uwezeshaji Kiuchumi kutoka TAMWA-ZNZ, Zaina Abdalla Mzee, amesema kuwa uwezeshaji wa kiuchumi kwa watu wenye ulemavu haupaswi kuishia katika kuwapatia ujuzi wa uzalishaji pekee, bali unapaswa kujumuisha pia maarifa ya biashara, utafutaji wa masoko na kuongeza thamani ya bidhaa ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Ameeleza kuwa vikundi vya KIJALUBA iSave tayari vimeanza kuzalisha bidhaa mbalimbali baada ya kupata mafunzo ya ujuzi wa uzalishaji, hivyo mafunzo haya ni hatua muhimu ya kuwasaidia kutambua fursa za masoko, kupanua wigo wa wateja na kuendesha biashara zao kwa ufanisi na uendelevu.
Kwa upande wake, mkufunzi wa masuala ya masoko na fedha kutoka Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Zainab Jabir Daudi, amesisitiza umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa, akieleza kuwa wafanyabiashara wanaweza kuwafikia wateja wengi zaidi kwa kutumia picha zenye mvuto, maelezo sahihi ya bidhaa na mawasiliano ya uhakika. Pia amewahimiza wanavikundi kushiriki katika maonesho ya biashara ili kutangaza bidhaa zao na kujenga mahusiano na wateja pamoja na wafanyabiashara wengine.
Akizungumzia mafunzo hayo, mmoja wa washiriki Asya Nassor Mwenyekiti wa Kikundi cha KIJALUBA cha Nia njema amesema: “Mafunzo haya yametufungua macho kuhusu namna ya kuboresha bidhaa zetu, hasa katika ufungashaji na utangazaji kupitia mitandao ya kijamii. Tunaamini maarifa tuliyoyapata yatatusaidia kuwafikia wateja wengi zaidi, kuongeza mauzo na kukuza biashara zetu.”
Naye Afisa Muwezeshaji kutoka TAMWA-ZNZ, Muhidini Ramadhan, amewahimiza washiriki kutumia maarifa waliyoyapata katika kuboresha shughuli zao za uzalishaji na biashara, akibainisha kuwa matumizi ya ujuzi wa vitendo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa kiuchumi na kujenga mazingira ya kujitegemea.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwezeshaji wa kiuchumi wa vikundi jumuishi vya KIJALUBA iSave, kwa kuhakikisha wanachama wanakuwa na uwezo si tu wa kuzalisha bidhaa, bali pia kuzitangaza, kuzipatia masoko na kuziuza kwa tija. Mafunzo hayo yameendeshwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na SHIJUWAZA, ZANAB na NAD kupitia Programu ya CADiR.
