JUMUIYA ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) vinalipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kuharakisha uchunguzi na kupatikana kwa mtuhumiwa wa kesi ya mauaji ya marehemu Khairat Juma Bakari ambae aliuawa kikatili katikati ya mwezi wa Mei, 2023.
Wiki iliyopita, Jeshi la Polisi Zanzibar lilitoa taarifa ya kukamatwa kwa mtuhumiwa Yusuf Ame Abubakar ambaye anatuhumiwa kwa mauaji ya Khairat Bakar yaliyotokea huko Mbuzini wilaya ya Magharibi “A” Unguja na kuripotiwa na vyombo vya habari tarehe 20 ya mwezi Mei 2023.
ZAFELA na TAMWA-ZNZ inapenda kulishukuru Jeshi la Polisi kwa hatua hiyo muhimu na kuendelea kuliomba jeshi hilo kuharakisha pia uchunguzi wa mauaji ya marehemu Laura Msemwa yaliyotokea katika tarehe hizo hizo ili mtuhumiwa aweze kupatikana na kufikishwa katika vyombo vya sheria ili kulipia makosa yake.
Aidha, ZAFELA na TAMWA ZNZ vinaviomba vyombo vya sheria vinavyofuata kuharakisha upatikanaji wa haki ya kijinai, na kutolewa hukumu stahiki kwa watuhumiwa watakaopatikana ili iwe funzo kwa wahalifu wengine ambao wana nia ovu ya kufanya vitendo vya kikatili kwa wanawake, watoto na jamii kwa ujumla.
TAMWA ZNZ na ZAFELA inatoa wito kwa jamii kuendelea kutoa mashirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kuwasaka wahalifu mbalimbali wa makosa ya jinai ili iwe rahisi kupatikana kwa wahalifu hao wa kesi hizo na hatimae kupunguza ama kumaliza matukio ya kihalifu hapa visiwani Zanzibar.
Tunaliomba Jeshi la Polisi kuendeleza utaratibu huu wa kutoa taarifa za hatua kwa hatua zinazofikiwa katika upelelezi wa makosa mbali mbali ya uhalifu dhidi ya wanawake & watoto na jamii kwa ujumla, kwani itasaidia sana kwa jamii kupata moyo zaidi na kujenga imani kwa Jeshi hilo na kuendelea kutoa mashirikiano na hatimae kupatikana kwa wahalifu.
Imetolewa na ZAFELA na TAMWA ZNZ.
Jamila Mahmoud Dkt. Mzuri Issa
Mkurugenzi Mkurugenzi
ZAFELA. TAMWA, ZNZ.
======================================================================