Edit Content

About Us

TAMWA is a national level Non-Governmental Organization known as Tanzania Media Women’s Association formed in 1987. TAMWA Zanzibar became fully self-governing and operational in both Isles of Unguja and Pemba since 2004. In January 2007, it attained its own separate registration.

Contact Info

Wanawake wenye nia ya kugombea Uchaguzi mkuu 2025 watakiwa kujifunza kwa waliowatangulia

KATIKA kuhakikisha ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi unaongezeka, wanawake wenye ndoto za kugombea uongozi wameshauriwa kuanza kujifunza kutoka kwa wanawake wanasiasa waliowatangulia ili kuongeza ujasiri na uthubutu wa kukabiliana na vikwazo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.

Ushauri huo umetolewa na wanasiasa wanawake wakongwe katika mkutano wa jukwaa la wanawake na uongozi lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari WanawakeTanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) na Ubalozi wa Norway kwa lengo la kuwaunganisha wanawake wanasiasa kutoka vyama mbalimbali vya siasa Pemba kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo kuhusu ushiriki wao kwenye nafasi za uongozi na namna ya kukabiliana na vikwazo vinavyoweza kurejesha nyuma ufikiaji wa malengo ya wanawake kiuongozi.

Mwana Masoud Ali, mbunge na mwakilishi mstaafu wa chama cha Wananchi CUF jimbo la Mtambwe Pemba, alisema ili wanawake wenye nia ya kugombea waweze kufanikiwa kiuongozi  ni lazima watenge muda kujifunza kutoka kwa wanawake waliowatangulia kuwaelekeza namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanawake wengi wanapojitokeza kugombea.

Alifahamisha kuwa wanawake wanapojitokeza kugombea nafasi za uongozi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kwenye jamii kutokana na mfumo dume uliojengeka hivyo inahitaji utayari wa wanawake kujiandaa mapema kukabiliana na vikwazo hivyo bila kukata tamaa.

Alitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wanawake kuwa ni rushwa, mitazamo hasi ya jamii kuhusu maadili na uwezo wa wanawake kwenye uongozi hivyo ni lazima wanawake wenye nia ya kugombea kujitayarisha mapema kukabiliana na mazingira ya vikwazo hivyo.

“Unapokuwa kiongozi, kwanza unatakiwa ujipe shimo ya nafsi yako, pili uheshimu mdomo wako na tatu uwe mvumilivu wa hali ya juu kwasababu sio wote watakupenda. Kila wakati unatakiwa uwe chini ya wanachi wako na ubadilike kadri ya matakwa yao,” alieleza Mwanasiasa huyo.

Aliongeza iwapo wanawake wenye nia ya kugombea kwenye uchaguzi mkuu 2025 watashirikiana na wanasiasa wanawake waliowatangulia itawasaidia kuwaongezea ujasiri na kuwapa mbinu zitakazowawesha kushinda katika uchaguzi huo bila kukubali kutumiwa kwa kuwanufaisha wengine.

Nae Lela Nassor Khamis, mbunge msitaafu Jimbo la Chonga kupitia chama ca Mapinduzi (CCM) alitaja heshima na kujithamini kuwa ni nguzo muhimu kwa mwanamke anapohitaji kugombea uongozi ili kutotoa nafasi kwa jamii kuchukulia kasoro hizo kama sababu zya kukosa Imani na uwezo wa wanawake kwenye uongozi.

Alifahamisha, “mwanamke ukiwa kiongozi lazima ujiheshimu, unatakiwa uthamini uanauke wako, ukijithamini hakuna mtu yeyote ataweza kukuvunjia heshima pale unapohitaji kuwa kiongozi. Na hayo yote unatakiwa kuanza kuyaonesha kwa jamii yako kuanzia sasa na sio kusubiri uchaguzi umefika.”

Katika hatua nyingine alipongeza juhudi za TAMWA Zanzibar kuona umuhimu wa kuanza kuwajengea uwezo wanawake wenye malengo ya kugombea katika uchaguzi mkuu kwani itasaidia kuwatayarisha kujitambua na kujua wajibu wao kama viongozi kabla ya kugombea.

“Nimefurahi kuona kwamba TAMWA Zanzibar inatoa mafunzo kwa wanawake na kuwapika kwaajili ya kuwa viongozi, naimani mafunzo haya yatatusaidia kuwa wanawake viongozi wazuri kwasababu huwezi kuwa kiongozi bora kama huna elimu ya nani kiongozi bora na unapaswa kufanya nini kama kiongozi, lakini pia yatanatujenga kuwa tayari kukabiliana na vikwazo vyote wakati wa kugombea,” alieleza.

Stara Khamis, ambaye ni mwanasiasa mwenye nia ya kugombea alisema fursa wanayopata wanawake kutoka TAMWA ZNZ ya kuelimishwa namna ya kujiandaa kugombea nafasi za uongozi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 imemwezesha kuwafikia wanawake wengine na kuwahamasisha kuwa tayari kugombea nafasi mbalimbali ili kuongeza ushiriki wao katika vyombo vya maamuzi.

Alieleza, “tangu nianze kupata mafunzo na kujengewa uwezo wa kugombea, nimeamua kutumia elimu hiyo niliyopata kuwahamasisha wanawake wengine hasa vijana wa kike. Nashukuru mpaka sasa nimewahamasisha vijana 45 wa kike katika wadi yangu ya Madungu waweze kujitoa na kuondoa hofu kuhusu kugombea uongozi kwasababu wanawake wengi wanakuwa na hofu kuingia katika uongozi hasa vijana kutokana na kukosa misingi na elimu sahihi ya uongozi.”

Aliongeza, “TAMWA inatupa mwelekeeo na njia ya kufikia malengo yetu wanawake katika uongozi. Ni jukumu letu sasa wanawake tusiangushe juhudi zao bali tuingie katika uongozi ili tufikie malengo mazuri ya usawa wa kijinsia kwenye vyombo vya maamuzi.”

Mapema mratibu wa TAMWA ZNZ ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said, aliwataka wanasiasa wanawake kutumia fursa ya kukutanishwa na wanasiasa wakongwe kujifunza na kupata uzoefu utakaowasaidia kujenga ujasiri wa kukabiliana na vikwazo wakati wa kugombea.

Alifahamisha kwamba TAMWA ZNZ kupitia mradi wa SWIL kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway imeamua kuandaa jukwaa la kuwaweka pamoja wanawake wanasiasa wapate fursa ya kujengeana uwezo na kuongeza mashirikiano kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 ili kujiandaa kikamilifu dhidi ya changamoto zinazowakabili wagombea wanawake kwenye chaguzi.

Mkutano huo ni utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake kudai haki zao na kushiriki katika uongozi (SWIL Project) unaotekelezwa na TAMWA ZNZ, PEGAO, ZAFELA kwa mashirikiano na Ubalozi wa Norway Tanzania.

———————MWISHO————–

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Subscribe to our
News and Presses

***We Promise, no spam!

A national level Non-Governmental Organization known as Tanzania Media Women’s Association formed in 1987.The registration number is 493 under Zanzibar Society Act No. 6 of 1995

We’re Available

Monday : 08.00 - 10.00
Tuesday : 08.00 - 10.00
Wednesday : 08.00 - 10.00
Thursday : 08.00 - 10.00
Friday : 09.00 - 07.00
Saturday : 10.00 - 05.00
Sunday : 10.00 - 05.00