CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAZELA) na Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) kupitia mradi wa kuinua Wanawake na Uongozi, wanatangaza tunzo maalum ya uandishi wa habari za Takwimu za wanawake na uongozi ikiwa ni katika maadhimisho ya kuelekea siku ya wanawake duniani ambayo kitaifa huadhimishwa kila ifikapo machi 8 duniani kote.
Tunzo hizo ni muendelezo wa shughuli zinazofanywa na mradi wa kuinua wanawake na uongozi kufikia 50/50 katika ngazi zote kupitia tasnia ya habari, kwa kuwashajiisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari ikiwa na lengo la kutumia vyombo vya habari katika kushajiisha masula ya wanawake na uongozi na kutanabahisha jamii na Taifa kwa ujumla umuhimu wa wanawake kuwemo katika nafasi za uongozi ili kukuza na kuimarisha demokrasia.
Tunzo hii itahusisha kazi zilizotolewa katika vyombo vya habari vya aina nne (4) kama ifuatavyo:
Uandishi wa habari za Makala katika magazeti (feature articles)
Uandishi wa habari wa vipindi katika redio (radio program)
Uandishi wa habari katika Televisheni (TV program)
Uandishi wa habari wa makala katika mitandao ya kijamii (feature articles in social media story).
Hivyo, TAMWA ZNZ na washirika wake inawaalika waandishi wa habari kukusanya kazi zao au kuandika katika eneo hilo na kuziwasilisha kwa wakati.
Vigezo muhimu vya kuzingatia wakati wa kuandaa au kuwasilisha habari ni:
Ubora wa kazi iliyowasilishwa
Upekee wa mada
Umuhimu wa kuzingatia uwiano sawa wa jinsia.
Vyanzo vingi vya habari vilivyojitawanya.
Ubunifu wa mada husika.
Matokeo baada ya kutoka habari au kipindi hicho (impact)
Uwasilishaji wa mada husika
Mpangilio wa mada
Ufasaha na mtiririko wa lugha
Kuzingatia maadili ya uandishi wa habari
Uweledi na matumizi ya TAKWIMU.
Kipindi cha Redio na Television kisizidi dakika 30 na pia sauti na picha ziwe katika ubora unaostahiki.
Kipindi au makala iliyochapishwa au kurushwa HEWANI katika vyombo mbali mbali vya habari vikiwemo magazeti, runinga, redio na mitandao ya kijamii katika kipindi cha kuanzia Januari 1 hadi Disemba 31, 2023.
Kazi ziwasilishwe katika ofisi ya Chama cha ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ) Tunguu karibu na IPA na Kwa Pemba kazi ziwasilishwe katika ofisi ya Tamwa Chake chake Pemba.
Hii ni mara ya tatu kufanyika tunzo ya aina hii ambapo mwaka jana jumla ya waandishi kumi walishinda tunzo za umahiri kwa upande wa magazeti na mitandao ya jamii.
Hata hivyo imebainika kuwa katika kufanyika kwa tunzo hio kuna changamoto na mafanikio kadhaa yaliyojitokeza.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na:
Waandishi kuzingatia zaidi kuandika makala na vipindi ambavyo ni vya matukio ambavyo vimekuwa vinawalenga zaidi viongozi au matokeo ya semina na mikutano.
Kuandika makala au vipindi ambavyo havikuwa na vyanzo tofauti vya habari na hivyo kukosa maoni ya watu wengi zaidi.
Makala hazikuwa na mvuto au mtiririko maridhawa na hivyo kukosa ubunifu na kuzifanya hazivutii.
Makala na vipindi havikuzingatia makundi mengine ya pembezoni wakiwemo walemavu, wanawake na wale wanaoishi vijijini.
Uwepo na ushiriki mdogo sana katika vipindi vya Televisheni.
Makala na vipindi vya habari vya uchunguzi wa kina vilikuwa navyo ni vichache sana.
Picha na sauti katika vipindi vya redio na Televisheni havikuwa katika ubora na baadhi vilikuwa havifunguki.
Hata hivyo pamoja na changamoto hizo bado kulikuwa na mafanikio:
Kuibua vipaji vya waandishi chipukizi na kuonekana ni kwa jinsi gani waandishi hao wamejitahidi katika kuweza kufikia viwango vinavyotakiwa.
Ushiriki wa waandishi wengi zaidi ambao wako katika rika tofauti chipukizi na wazoefu.
Mashirikiano ya pamoja kwa wadau wa habari na kuzifanya tunzo hizi kuwa na mvuto na kuzitangaza kwa kina.
Mwisho katika kuimarisha kada ya habari tunatoa wito maalum kwa wanahabari kujiendeleza zaidi katika fani na pia kutoa wito maalum kwa taasisi za habari pamoja na vyombo vya habari kuimarisha mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa waandishi wa habari.
Waandishi wa habari tufahamu kuwa kazi hii ni kusaidia jamii na hivyo ni muhimu kutumia kalamu na vipaaza sauti katika kuelimisha na kuibua kero na sauti za wasio na sauti.
Ni muhimu kwa waandishi na wahariri kuimarisha kada hii kwa kufuata kwa vitendo maadili ya habari lakini wito kwa wahariri kuwasaidia waandishi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Natoa shukuran kwa waandishi kwa kuendelea na majukumu yao na kutoa wito kwa ushiriki zaidi katika mashindano haya kwa lengo la kuimarisha kada ya habari lakini pia katika kuandika habari za takwimu za wanawake na uongozi.
“KALAMU YANGU MCHANGO WANGU KWA WANAWAKE”.
Imetolewa na:
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ)
Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA)
Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO)