JUMLA ya kazi 529 za waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari zimewasilishwa kwa ajili ya kuwania tuzo za umahiri za uandishi wa habari za takwimu za wanawake na uongozi.
Miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na vipindi vya redio, televisheni, makala za magazeti na zile kutoka katika mitandao ya kijamii zilizoandikwa na kurushwa katika vyombo vyao kuanzia mwezi Janauari hadi Disemba 31, 2023.
Kazi hizo zinaonesha ni jinsi gani waandishi wamekuza mwamko wa kuandika habari za uongozi kwa wanawake ambapo zinashajihisha wanawake na vijana wakike kujiamini zaidi na kuwa na matumaini ya kupata nafasi mbali mbali za uongozi lakini pia zinaielimisha jamii kuhusu umuhimu wa wanawake katika uongozi.
Lengo la tuzo hizo ni kuhimiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao na vyombo vya habari kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa masuala ya wanawake katika uongozi na hivyo kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi mbalimbali za maamuzi.
Hii ni mara ya tatu kwa tunzo hizo kufanyika hapa Zanzibar na kwa mwaka huu zinatarajiwa kufanyika mapema mwezi Machi, 2024.
Tuzo za umahiri za uandishi wa habari za takwimu za wanawake na uongozi zinaandaliwa kwa pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar, (TAMWA – ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya inayojihusisha na Mazingira, Usawa wa Kijinsia, na Utetezi Pemba (PEGAO), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.
Dkt. Mzuri Issa,
Mkurugenzi,
TAMWA ZNZ.