7/11/2024
Jumla ya waandishi wa habari 30 wa Unguja na Pemba kutoka vyombo mbalimbali vya habari wamepatiwa mafunzo ya siku mbili kuweza kuandika kwa umahiri habari za wanawake na uongozi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Chama Cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Community Forest Pemba (CFP) na Community Forest International (CFI).
Akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa TAMWA-ZNZ Tunguu, Mkurugenzi wa Chama hicho Dkt Mzuri Issa amesema ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoongezeka kwa kasi, kuna umuhimu mkubwa wa kuwapa mafunzo waandishi wa habari ili waweze kuandika taarifa zenye kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.
Aidha Dkt Mzuri ameeleza kuwa, mikakati mbali mbali ya nchi, ya kikanda na dunia pamoja na sera na bajeti za serikali zimewekwa kukabiliana na changamoto hizo hivyo waandishi wanaweza kuzitumia kuelimisha jamii kupitia kazi mbali mbali ambazo wataziandaa.
‘’Ni ukweli usiopingika kuwa mabadiliko ya tabianchi ni makubwa na athari zake zinaonekana hata kwa hali ya kawaida, kama kubadilika kwa misimu ya mwaka, hunyesha mvua kubwa zinazosababisha mafuriko na kupanda kwa kina cha maji ya bahari”
Meneja Mawasiliano TAMWA- ZNZ Saphia Ngalapi amesema kupitia tathimini iliofanywa na TAMWA – ZNZ mapema mwezi wa September 2024 kuhusu habari zilizoandikwa juu ya masuala ya uongozi wa wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kipindi cha Januari- Mei 2024 ilikuwa ni ndogo ambapo waandishi wa habari walieleza kushindwa kuandika habari hizo kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Tathmini hiyo iliofanywa na TAMWA ZNZ chini ya mradi wa ZanzAdapt hivi karibuni imeonesha kuwa jumla ya habari 2,600 na vipindi 1,161 vya televisheni na redio vilivyopitiwa, ni vipindi 11 tu ambavyo ni sawa na asilimia 0.9 na habari 56 kati ya 2,600 ambazo ni sawa na asilimia 2.1 ndizo zilizoelezea wanawake na nafasi za uongozi kwenye mabadiliko ya tabianchi. Vilevile, kati ya magazeti 608 yaliyopitiwa, ni habari 34 tu sawa na asilimia 5.5 zilizohusu uongozi wa wanawake na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo Ali Nassor Sultan amesema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha athari kwa kila nyanja ikiwemo afya, uchumi mazingira na miundombinu, hivyo amewataka waandishi kuonesha athari hizo kwa ukubwa wake katika jamii na kuonyesha nafasi ya uongozi wa wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Community Forest Pemba (CFP) na Community Forest International (CFI) wanatekeleza mradi wa miaka miwili wa Uongozi wa Wanawake Zanzibar katika Uhimilivu (ZanzAdapt) wenye lengo la kuboresha usawa wa kijinsia na uwezo wa uhimilivu wa tabianchi unaotegemea mazingira katika jamii za pwani zilizo hatarini kwenye Visiwa vya Unguja na Pemba.