
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU TUZO ZA UANDISHI WA HABARI ZA TAKWIMU (DATA JOURNALISM AWARDS 2025)
Tarehe: 19 Mei 2025
Ndugu waandishi wa habari,
Napenda kuwashukuru kwa kuitikia wito wetu na kwa kazi kubwa mnayoendelea kufanya ya kuhabarisha umma na kuhamasisha mabadiliko chanya katika jamii yetu.
Leo, tunakutana hapa kuwajulisha rasmi kuhusu Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari za Takwimu – Data Journalism Awards 2025, ambazo zinatarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi, tarehe 24 Mei 2025, katika ukumbi wa Police, Ziwani – Zanzibar.
Tuzo hizi zinalenga kutambua na kuthamini kazi bora za waandishi wa habari na vyombo vya habari vinavyotumia takwimu kwa ufanisi kuandika habari zinazopaza sauti za wanawake na kuhamasisha usawa wa kijinsia, hasa katika nafasi za uongozi.
Kwa mwaka huu, tumeongeza kipengele maalum kwa ajili ya vyombo vya habari vyenyewe (media houses) kwa lengo la kutambua juhudi zao za ndani katika kuendeleza misingi ya usawa wa kijinsia.
Katika hatua hii, majaji wamekagua jumla ya vyombo tisa (9) vya habari kutoka Unguja na Pemba ili kutathmini utekelezaji wa misingi ya usawa wa kijinsia katika mazingira ya kazi, sera za ndani, nafasi za uongozi ndani ya chombo, na namna vyombo hivyo vinavyoweka ajenda za jinsia katika kazi zao za kila siku.
Kwa upande wa vyombo vya habari vitakavyokuwa vimefanya vizuri na kushinda, tutatoa alama ya kuthibitisha (stamp of approval) kuwa chombo hicho kinatekeleza kwa dhati misingi ya usawa wa kijinsia kwa ndani na nje.
Aidha, jumla ya kazi 235 za waandishi wa Habari kutoka Unguja na Pemba ziliwasilishwa kwa ajili ya mchakato wa ushindani. Kazi hizo zimegawanywa katika makundi manne (4) ya ushindani ambayo ni: Radio, Televisheni, Mitandao ya kijamii na Magazeti.
Kila kundi limepata usimamizi na uchambuzi wa kina kutoka kwa jopo la majaji waliobobea, wakitumia vigezo mahsusi kama vile matumizi ya takwimu, ushawishi wa habari, ubunifu, na mtazamo wa kijinsia.
Vilevile, tutakuwa na kipengele maalum cha kuwatambua waandishi wa habari vijana (YMF) waliobobea katika kuandika habari zenye muktadha wa kijinsia na takwimu. Hii ni sehemu ya kutambua juhudi za vijana 20 waliokuwa kwenye programu ya Waandishi kijana ya mwaka mmoja kuanzia Juni 2024 hadi Mei 2025.
Kupitia Waandishi kijana hiyo, vijana hao walipewa mafunzo ya nadharia na vitendo juu ya uandishi wa habari za jinsia, matumizi ya takwimu, na uandishi wa habari zenye athari kwa jamii. Katika tuzo hizi, baadhi yao watatambuliwa kwa umahiri wao katika kuandika habari zenye ubora, ubunifu, matumizi ya mitandao ya kijamii na mtazamo wa kijinsia unaoendana na malengo ya Tuzo hizi.
Tuzo hizi ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya Kuwawezesha Wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL), ambayo inatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiyay a Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) na Jumuiyay a Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), kwa ushirikiano na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.
Katika kipindi cha mwaka 2024/2025, tumeandaa Tuzo hii kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS) kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza utetezi wa uandishi wa habari unaozingatia matumizi ya takwimu ndani ya sekta ya habari.
Tunapokaribia siku hii muhimu ya Tuzo, tunawahimiza waandishi wa habari, wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari, mashirika ya kiraia, viongozi wa serikali na wananchi kwa ujumla kushiriki nasi katika tukio hili muhimu ambalo pia litakua mubashara (LIVE) katika baadhi ya vyombo vya habari.
Tukio hili si tu linatambua juhudi za waandishi na vyombo vya habari katika kuendeleza usawa wa kijinsia, bali pia linaweka msingi thabiti wa mustakabali wenye haki, usawa, na uwajibikaji katika tasnia ya habari na jamii kwa ujumla.
Imetolewa na:
TAMWA ZNZ, OCGS, JUWAUZA, PEGAO & ZAFELA.