
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAREHE: 17 AGOSTI, 2025
Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) inaiomba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)
kuhakikisha usalama wa Waandishi wa Habari, Wanawake wagombea, na Wasimamizi
wa Uchaguzi (Mawakala) katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi mkuu wa
Zanzibar ambao umeshatangazwa kuwa utafanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka
huu.
ZAMECO inatambua kuwa mazingira salama kwenye masuala muhimu yenye maslahi
mapana na mustakabali wa nchi hususan hili la uchaguzi, ni sharti la msingi ili kuhakikisha
kila mdau anatekeleza majukumu yake kwa uhuru na bila ya hofu kama ilivyoelezwa
katika Ibara ya 15(1) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984:
“(Kila mtu anastahiki kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi
na ya nyumbani kwake, na pia heshima, na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano
yake).” Hivyo Kamati inasisitiza kuzingatiwa hatua mahsusi kwa mujibu wa sheria na
kanuni, za kulinda haki na usalama wa makundi haya wakati wa uchaguzi na baada ya
uchaguzi.
Kadhalika, Waandishi na jamii kwa ujumla, wapewe fursa ya kupata taarifa bila ya
kuingiliwa kwani kila mmoja ana haki hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya
Zanzibar 1984 sambamba na ibara ya 19 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binaadamu
(UDHR-1948) inayoeleza “Kila mtu ana haki ya kuwa na maoni na mawazo yake bila
kuingiliwa. Ana haki ya kushikilia maoni yake bila kuingiliwa, na pia haki ya kutafuta,
kupokea na kutoa habari na mawazo kwa njia yoyote ile na bila kujali mipaka”.Aidha ZAMECO inasisitiza pia umuhimu wa Waandishi wa Habari kupewa nafasi sawa
zisizo na ubaguzi katika kupata taarifa sahihi za uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kupatiwa
vitambulisho maalum vinavyotolewa na Tume ya Uchaguzi na kuepuka kutoa fursa zaidi
kwa vyombo vya Serikali na kuvikwepa vyombo visivyokuwa vya Serikali (vyombo vya
binafsi). Hii itawawezesha kufuatilia na kuripoti matukio ya uchaguzi kwa weledi, usawa
na bila ya kuathiriwa na vikwazo visivyo vya lazima.
Pia kamati inapendekeza Tume ya Uchaguzi kutoa mafunzo maalum kwa waandishi wa
habari kuhusu uandishi wa taarifa za uchaguzi kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, weledi
na maadili ya taaluma, ni matumaini yetu kwamba mafunzo haya yatasaidia kuimarisha
uelewa wa waandishi katika kuripoti kwa usawa kuhusu wagombea wanawake na
wanaume, na hivyo kuchochea ile dhana maarufu ya “ushiriki jumuishi” katika siasa.
Katika hatua nyengine, ZAMECO inapongeza ahadi iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar ya kutoa na kuchapisha takwimu za jinsia za washiriki wa uchaguzi, ikiwemo
idadi ya wanawake na wanaume watakaogombea nafasi mbalimbali (Urais, Uwakilishi na
Udiwani) pamoja na wapigakura na washiriki wa mchakato mzima wa uchaguzi ambapo
takwimu hizi zitakuwa nyenzo muhimu katika kufuatilia uwiano wa kijinsia na kusaidia
kufikia lengo la usawa wa asilimia 50/50 nchini.
ZAMECO inahitimisha kuwa uchaguzi huru, wa haki na jumuishi unahitaji mazingira
salama, taarifa sahihi, na upatikanaji sawa wa fursa kwa wanawake na wanaume, ili
kuimarisha demokrasia na mshikamano nchini.
MWISHO