WANAWAKE VIJANA WATAKIWA KUTUMIA MAFUNZO YA W-LEAD KUSHIKA NAFASI ZA UONGOZI

Wanawake vijana, wakiwemo wenye ulemavu, wametakiwa kutumia maarifa na ujuzi wanaoupata kupitia mafunzo ya mradi wa W-LEAD kwa kujiamini, kutimiza ndoto zao na kuongeza ushiriki wao katika nafasi za uongozi na maamuzi ili kuchangia maendeleo ya jamii.

Wito huo umetolewa na Mtaalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Mohamed Khatib Mohamed, kwa niaba ya Mkurugenzi wa chama hicho, Nairat Abdulla Ali, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne kwa viongozi wanawake vijana kutoka vyama vya siasa, asasi za kiraia na vyuo vikuu Zanzibar, yaliyofanyika katika ofisi za TAMWA-ZNZ, Tunguu, Unguja.

Mohamed amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki uwezo wa kiuongozi, kuimarisha kujiamini, kuboresha mawasiliano na kuwaandaa kushiriki kikamilifu katika nafasi mbalimbali za maamuzi. Ameeleza kuwa baada ya mafunzo, baadhi ya washiriki watapata fursa ya kujifunza kwa vitendo katika taasisi mbalimbali kwa kipindi cha miezi mitatu ili kutumia maarifa waliyopata katika mazingira halisi ya uongozi.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Salmin Amour Mohammed, amewataka wanawake vijana, hususan wenye ulemavu, kuthibitisha kwa vitendo uwezo wao wa kuongoza na kuondoa dhana potofu kwamba uongozi ni jukumu la wanaume pekee. Amesisitiza kuwa wanawake wanapaswa kufuatilia ndoto zao bila kukata tamaa na kutumia uwezo wao kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Kwa upande wake, Lulu Alai Abdallah, Katibu wa Wilaya ya Mjini wa UVCCM Zanzibar, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa misingi ya uongozi bora, kuboresha mawasiliano na kujenga ujasiri wa kuzungumza mbele ya watu. Ameongeza kuwa wanawake wana uwezo wa kufanya kazi katika sekta mbalimbali, zikiwemo uhandisi, udaktari na uongozi, hivyo wanapaswa kuondokana na mtazamo unaowafungia katika majukumu ya nyumbani pekee.

Washiriki wengine, Sabrina Faki Hamad kutoka Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Rahma Abeid Awadh kutoka Jumuiya ya Elimu Vijana Kaskazini Unguja na Bahati Ramadhan Hassan, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), wamesema mafunzo hayo yamewaongezea kujiamini, uelewa wa haki za wengine na uwezo wa kufanya maamuzi bila kubaguliwa kwa misingi ya jinsia au ulemavu. Wamesema wataitumia elimu hiyo kuhamasisha wanawake wengine kushiriki katika uongozi na kuwa mfano bora katika familia, vyuo na jamii kwa ujumla.

Mradi wa W-LEAD, unaotekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na UN Women pamoja na wadau mbalimbali, ukiwemo Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), SUZA, Jumuiya ya Watu Wasioona Zanzibar (ZANAB) na taasisi nyingine, unalenga kuimarisha ushiriki wa vijana katika uongozi, uwajibikaji na demokrasia. Mradi huo ulianza Machi 2026 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2027, ukiwa na lengo la kuwafikia vijana 50 katika awamu ya kwanza, wakiwemo wasichana 30 na wavulana 20, huku ukiendeleza juhudi za kukuza uongozi jumuishi na usawa wa kijinsia katika nafasi za maamuzi.

Kupitia mafunzo hayo, TAMWA-ZNZ inalenga kuona vijana wanatumia ujuzi wanaoupata kuleta mabadiliko katika jamii, huku wanawake na wasichana wakihamasishwa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi na kushiriki katika michakato ya maamuzi. Ushiriki huo unatarajiwa kusaidia kupunguza vikwazo vinavyowakabili wanawake, wakiwemo wenye ulemavu, na kujenga jamii inayotambua uwezo wa kila mtu katika kuleta maendeleo.

Subscribe to our
News and Presses

***We Promise, no spam!

A national level Non-Governmental Organization known as Tanzania Media Women’s Association formed in 1987.The registration number is 493 under Zanzibar Society Act No. 6 of 1995

We’re Available

Monday : 08.00 - 10.00
Tuesday : 08.00 - 10.00
Wednesday : 08.00 - 10.00
Thursday : 08.00 - 10.00
Friday : 09.00 - 07.00
Saturday : 10.00 - 05.00
Sunday : 10.00 - 05.00