TAMWA ZNZ YAWAPONGEZA TIMU YA WARRIOR QUEENS KUSHIRIKI MECHI YA KLABU BINGWA AFRIKA, ETHIOPIA
Watekelezaji wa program ya Michezo kwa Maendeleo (S4D) wanawatakia kila la kheri timu ya Warrior Queens ya Saateni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika kwa upande wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yanayotarajiwa kufanyika nchini Ethiopia kuanzia tarehe 17 mpaka tarehe 31 Agosti mwaka huu 2024.
Timu ya Warrior Queens itaiwakilisha Zanzibar katika mashindano hayo na inatarajiwa kuondoka nchini kuelekea Ethiopia siku ya Alkhamis, tarehe 15 Agosti 2024. Tunaamini kuwa wataiwakilisha Zanzibar kwa fahari kubwa na kurudi nyumbani wakiwa washindi.
Pamoja na kuwapongeza wadau wote waliofanikisha timu hii kukamilisha mahitaji ya safari hiyo, TAMWA ZNZ inasisitiza umuhimu kwa wadau wote kuendeleza usawa wa kijinsia kwa kuzisaidia timu za wanawake na kukuza vipaji vyao ili kujenga jamii inayothamini na kuinua michango ya wanawake.
Bado ipo haja kwa wadau wote wa michezo, ikiwemo serikali, taasisi binafsi, na wadau wengine, kuongeza nguvu katika kuzisaidia timu za wanawake ili kuwawezesha wachezaji wetu wa kike kushiriki na kushinda mashindano mbalimbali, ndani na nje ya nchi.
Kufuzu kwa klabu ya WARRIOR QUEENS kwenye mashindano hayo kunatokana na klabu hiyo kuchukua ubingwa wa ligi kuu soka Zanzibar upande wa wanawake msimu wa 2023 2024 ambapo jumla ya timu 10 za wanawake zilishiriki.
Program ya S4D inatekelezwa kwa mashirikiano na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD) kwa mashirikiano makubwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Ujerumani (GIZ).