Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA – ZNZ) Dkt Mzuri Issa amewataka wahariri wa vyombo vya habari kutumia kalamu zao kushawishi mamlaka zinazohusika na mapitio ya Sheria na Sera za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kufanya kazi ipasavyo ili kupunguza changamoto zinaweza kuepukika.
Dkt Mzuri amesema hayo katika mkutano wa kuwajengea uwezo Wahariri wa vyombo vya habari
Zanzibar kuzipa kupaumbele habari zinazohusu nafasi ya uongozi kwa mwanamke katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mradi wa (ZANZIADAPT) uliofanyika katika Ofisi za chama hicho Tunguu Mkoa wa kusini Unguja.
Ameeleza kuwa wanawake wanafanya jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ila bado hawafikiwi ipasavyo na vyombo vya habari, hivyo amewaomba wahariri kutumia nafasi hiyo kuhakikisha sauti za wanawake zinasikika.
Afisa kutoka Community Forest Pemba (CFP) Zulpha Mbwana amesema lengo la mradi wa huu ni kuongeza nafasi ya uongozi kwa wanawake na kuinua sauti zao zisizosikika ipasavyo kupitia vyombo vya habari katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akiwasilisha mada kuhusu jinsia na mabadiliko ya tabianchi, Mwandishi mwandamizi Issa Yussuf amesema wanawake wanajitoa kuhudumia jamii kama vile kutafuta kuni, maji na kulea familia hasa maeneo ya vijijini hivyo wanapata shida kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na mazingira yaliyowazunguka.
Nao wahariri kutoka vyombo vya habari Zanzibar wamesema wataifanyia kazi kwa vitendo kwa elimu hio waliopatiwa na TAMWA-ZNZ kwa kuhariri na kuchapisha habari hizo sambamba na kuwa msatari wa mbele kuhakikisha zinapata nafasi katika vyombo vyao.
Mradi wa ZANZIADAPT ni wa miaka miwili ambao unatekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Community Forest Pemba (CFP) na Community Forest International ambao umelenga kutekelezwa Shehia ya Uzi, Uzi Ng’ambwa, Bungi na Unguja Ukuu kwa upande wa Unguja na Shehia ya Kambini, Mjini Kiuyu, Chwale na Mchanga mdogo kwa Pemba.