
@TAMWA_Zanzibar www.tamwaznz.or.tz
30 Machi 2025
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMWA ZNZ YAITAKA JAMII KUCHUKUWA TAHADHARI NA KUWALINDA
WATOTO KIPINDI CHA SIKUKUU YA EID-EL-FITRI
Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ)
kinatoa wito kwa wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla kuchukua tahadhari ya hali ya
juu katika kuhakikisha usalama wa watoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji, hasa
wakati huu wa sherehe za Sikukuu ya Eid El Fitri inayofanyika baada ya kumalizika
mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
TAMWA ZNZ inasisitiza kuwa ni muhimu kwa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba
watoto hawatoki peke yao kwenda sikukuuni, ili kuepuka matukio ya udhalilishaji
ikiwemo kubakwa, kulawitiwa, kutoroshwa pamoja na kupotea kwa watoto ambapo
matukio haya mara nyingi hutokea katika viwanja mbalimbali vya kufurahishia watoto.
Aidha chama kinaiomba jamii kuzidisha umakini na kuwapa uangalizi wa karibu watoto
ikiwemo kuacha tabia ya kuwapa dhamana watoto kuwa viongozi wa watoto wenzao,
kufanya hivyo kunapelekea udhibiti na usalama mdogo wa watoto na kupelekea urahisi
wa kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
Takwimu za vitendo vya udhalilishaji kwa mwaka 2024 zilizotolewa na Ofisi ya
Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaonesha kuwa kati ya waathirika
1809 wa vitendo hivi, watoto walikua ni 1525 sawa na asilimia (84.3%), hivyo watoto
wapo katika hatari kubwa ya kukumbwa na vitendo vya udhalilishaji na ukatili.
Vilevile TAMWA ZNZ inawataka wazazi na walezi kuvunja ukimya kwa kuzungumza na
watoto na vijana wao kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, kujitambua na
kujiepusha na mapenzi ya mapema ili waweze kusoma na kutimiza ndoto zao.
Aidha, TAMWA ZNZ inatoa wito kwa taasisi zinazosimamia sheria kuendelea kufanya
kazi kwa uadilifu ili kutokomeza vitendo vya udhalilishaji na kuhakikisha haki za watoto
zinaheshimiwa na kulindwa.
Mwisho kabisa, TAMWA ZNZ inawatakia wazanzibari wote sherehe njema za sikukuu
ya Eid El Fitri na inasisitiza umuhimu wa kuwa na amani na umoja ili kwa pamoja
tuweze kulinda haki za wanawake na watoto.
CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI WANAWAKE
TANZANIA
P. O. Box 741 Tunguu Zanzibar, TEL: 0242232263
Mobile No. 0772378378
Email: info@tamwaznz.or.tz
@TAMWA_Zanzibar www.tamwaznz.or.tz