Wanawake wagombea wapatiwa mafunzo ya kujiamini kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Dkt. Mzuri Issa Ali, amesema changamoto wanazokutana nazo wanawake wanapogombea nafasi za kisiasa ni pamoja na kukatishwa tamaa na udhalilishaji wa kijinsia. Amesisitiza kuwa sasa ni wakati muafaka kwa wanawake kuvuka vikwazo hivyo na kuchukua nafasi za uongozi majimboni na kitaifa.
Dkt Mzuri amesema jamii inapowaona wanawake wenye uthubutu na uwezo wa kuongoza huonesha dharau kwa lengo la kuwavunja moyo na kuwarudisha nyuma. Ni muhimu wanawake kuungana, kushirikiana na kushikamana ili kuondoa mfumo dume na kufikia usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50 katika uongozi wa kisiasa.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya siku tatu yaliyohusisha wanawake wagombea 56 kutoka vyama 18 vya siasa kwa upande wa Unguja katika mafunzo yaliandaliwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na PEGAO, JUWAUZA na ZAFELA, kwa lengo la kuwajengea ujasiri, kuwapa mbinu za kukabiliana na changamoto na kuendesha kampeni kwa ubora katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano wa TAMWA-ZNZ, Saphia Ngalapi, akitoa mada kuhusu matumizi sahihi ya vyombo vya habari, aliwataka wagombea hao kutumia ipasavyo majukwaa ya habari na mitandao ya kijamii katika kunadi sera zao.
“Vyombo vya habari ni nyenzo muhimu inayowawezesha wagombea kufikisha ujumbe kwa haraka na kwa uwigo mpana, sambamba na mitandao ya kijamii ni jukwaa linalofuatiliwa na wapiga kura wengi, hivyo ni muhimu kuitumia kwa ubunifu katika kunadi sera zao,” alisema Ngalapi.
Akiwasilisha mada kuhusu mbinu za kushawishi wapiga kura, Mkufunzi Dkt. Salum Suleiman Ali aliwataka wanawake wagombea kujiamini, kuandaa sera zenye mashiko na zinazotekelezeka sambamba kuonesha uwezo wao katika kunadi sera kwa umakini ili kuvutia wapiga kura wengi.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Asiata Saidi Abubakar aliishukuru TAMWA-ZNZ kwa kuandaa mafunzo hayo na kueleza kuwa yamewaongezea uelewa na mbinu za kujilinda, kujiamini na kutumia vyombo vya habari kwa ufanisi.
“Maarifa tuliyoyapata yatatupa ujasiri na uthubutu wa kusimama imara katika kampeni, kuongeza idadi ya wapiga kura na kuchangia kufanikisha lengo la kufikia uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50 katika nafasi za uongozi,” alisema.
Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa viongozi wanawake ni waadilifu, wachapakazi, na wenye kujali masuala ya jamii kwa umakini mkubwa. Wanawake mara nyingi hupendelea mazungumzo na maridhiano badala ya migogoro, jambo linaloleta mshikamano na manufaa kwa jamii nzima.
Mafunzo kama haya yaliandaliwa kisiwani Pemba, ambapo jumla ya washiki 30 kutoka vyama vya siasa 10 walishiriki.
Mafunzo haya ni sehemu ya program ya kukuza ushiriki wa wanawake katika uongozi na siasa ambayo yameandaliwa kwa pamoja na Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba (PEGAO) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA Zanzibar) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.
