TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMWA-ZNZ YATANGAZA TUZO ZA CHAMPION DATA JOURNALISM 2026–2027
Kuongeza wigo wa uandishi wa habari unaotumia takwimu na ushahidi zanzibar
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), kinatangaza kuendelea kwa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari za Takwimu (Champion Data Journalism Awards) 2026–2027, zinazolenga kutambua, kuhamasisha na kuenzi waandishi wa habari wanaoonesha ubora katika matumizi ya takwimu, ushahidi, uchambuzi na ubunifu katika kuandika habari zinazogusa masuala muhimu ya kijamii, kiutawala na kimaendeleo Zanzibar.
Tuzo hizi ni sehemu ya jitihada za TAMWA-ZNZ za kuimarisha uandishi wa habari wenye tija kwa umma, unaokwenda zaidi ya kuripoti matukio ya kawaida na badala yake kutumia taarifa, tafiti, takwimu na ushahidi kuibua changamoto za jamii, kuimarisha mijadala ya umma na kuwaajibisha wenye dhamana ya kufanya maamuzi.
Msimu wa sita unaashiria hatua mpya katika maendeleo ya tuzo hizi. Kwa takribani miaka mitano mfululizo, Tuzo hizi zimekua zikitekelezwa kupitia Programu ya Kuimarisha Uongozi kwa Wanawake (SWIL) kwa ushirikiano na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania (RNE).
Baada ya kukamilika kwa programu ya SWIL, TAMWA-ZNZ imeamua kuendeleza na kukuza Tuzo hizi kuwa jukwaa endelevu linaloshirikisha wadau mbalimbali wenye dhamira ya kuimarisha ubora na matokeo ya uandishi wa habari Zanzibar.
Kwa nini Tuzo za Champion Data Journalism?
Vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuhabarisha umma, kuwezesha upatikanaji wa taarifa, kuimarisha mijadala ya kijamii na kuibua masuala yanayohitaji uwajibikaji. Hata hivyo, bado kuna changamoto katika uchambuzi wa kina, matumizi ya takwimu na ufuatiliaji wa masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya jamii.
Ripoti ya mwaka 2025 ya Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO), ilibaini kuwa kati ya Habari 901 zilizoandikwa ni habari 12 pekee ndizo zilizokuwa za uchunguzi.
Vilevile, Tathmini ya Kihabari Kuhusu Wanawake na Mabadiliko ya Tabianchi iliyofanywa mwaka 2024 na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Community Forest Pemba na Community Forest International, ilibaini kuwa kati ya matoleo 608 ya magazeti yaliyopitiwa, ni makala 34 pekee zilihusu uongozi wa wanawake na mabadiliko ya tabianchi. Matokeo haya yanaonesha umuhimu wa kuongeza uandishi unaozingatia sauti za wanawake, usawa wa kijinsia na matumizi ya takwimu katika kuibua masuala yanayoathiri jamii.
Kwa msingi huo, Tuzo za Champion Data Journalism zinalenga kuhamasisha waandishi kutumia takwimu na ushahidi katika kuandaa habari zenye kina, zinazojenga uelewa wa umma na kuchangia uwajibikaji pamoja na mabadiliko chanya katika jamii.
Makundi ya Tuzo
Katika Msimu wa mwaka 2026/2027, Tuzo zitazingatia maeneo sita muhimu yafuatayo:
Uongozi wa Wanawake: Kutambua habari zinazoangazia ushiriki, mafanikio, changamoto na mchango wa wanawake katika uongozi, utawala, siasa na michakato ya kufanya maamuzi.
Elimu: Kuhamasisha uandishi unaochunguza upatikanaji na ubora wa elimu, ushiriki wa wanafunzi, miundombinu ya elimu na elimu jumuishi.
Ukatili wa Kijinsia (GBV): Kutambua habari zinazochunguza ukatili wa kijinsia, sababu na athari zake, kinga, upatikanaji wa haki na hatua zinazochukuliwa na taasisi husika, kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.
Haki na Ushirikishwaji wa Watu wenye Ulemavu: Kuimarisha uandishi unaoonesha haki, ushirikishwaji na ushiriki sawa wa watu wenye ulemavu katika elimu, ajira, uongozi, uchumi, na maeneo mengine ya kijamii.
Uhuru wa Kujieleza: Kuhamasisha uandishi unaochangia uelewa kuhusu uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa taarifa, uhuru wa vyombo vya habari, usalama wa waandishi wa habari na ushiriki wa wananchi katika masuala ya umma.
Mabadiliko ya Tabianchi: Kutambua habari zinazotumia takwimu, ushahidi na ubunifu kuangazia mabadiliko ya tabianchi, changamoto za mazingira na athari zake kwa jamii.
Nani Anaweza Kushiriki?
Tuzo hizi zitawalenga waandishi wa habari binafsi kutoka Unguja na Pemba wanaofanya kazi katika vyombo vya habari vya magazeti, redio, televisheni na majukwaa ya mtandaoni.
Vigezo vya Tathmini
Kazi zitakazowasilishwa zitapimwa kwa kuzingatia ubora na upekee wa mada, matumizi sahihi ya takwimu na vyanzo vya kuaminika, uchambuzi wa kina, ubunifu katika uwasilishaji, umuhimu wa mada kwa jamii, uzingatiaji wa maadili ya uandishi wa habari, ushirikishwaji wa mitazamo mbalimbali na uwezo wa kazi husika kuchochea uelewa, uwajibikaji na mabadiliko chanya.
Tathmini itafanywa na jopo la majaji wenye utaalamu, uzoefu na uadilifu katika maeneo husika ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi wa washindi unazingatia weledi, uwazi na usawa.
Muundo wa Tuzo na Utambuzi wa Washindi
Kupitia maeneo sita ya tuzo, washindi watatu watatambuliwa kila eneo, ambao ni mshindi wa kwanza, mshindi wa pili na mshindi wa tatu.
Shughuli ya utoaji wa tuzo imepangwa kufanyika Mei 8, 2027, na inatarajiwa kuwakutanisha washiriki takribani 200, wakiwemo waandishi wa habari, wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari, Serikali, asasi za kiraia, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na wadau wengine.
Ushirikiano wa Wadau
Katika hatua hii mpya, TAMWA-ZNZ inalenga kupanua ushirikiano na taasisi za Serikali, asasi za kiraia, washirika wa maendeleo na sekta binafsi ambazo majukumu yao yanahusiana na maeneo sita ya Tuzo.
Taasisi ambazo zimeonesha nia ya kushirikiana na TAMWA-ZNZ katika utekelezaji wa toleo hili ni pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Jumuiya ya Norway ya Watu Wenye Ulemavu (NAD) na Muungano wa Mashirika ya Kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (ZACCA). TAMWA-ZNZ pia itaendelea kuwashirikisha wadau wengine wenye taaluma na dhamira ya kuimarisha uandishi wa habari wenye maslahi kwa umma.
Ushirikiano huu unalenga kuimarisha utekelezaji na uendelevu wa tuzo kupitia upatikanaji wa utaalamu na maarifa ya kitaalamu, takwimu na taarifa sahihi, ushauri wa kitaalamu katika mchakato wa majaji, pamoja na kuongeza mwonekano wa tuzo na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali na fursa mbalimbali zitakazochangia mafanikio yake.
Hitimisho
Tuzo za Champion Data Journalism 2026/2027 ni zaidi ya kutambua kazi bora za waandishi wa habari; ni uwekezaji katika kuimarisha nafasi ya vyombo vya habari kama chombo cha kuhabarisha, kuelimisha, kuibua changamoto na kuimarisha uwajibikaji katika jamii.
TAMWA-ZNZ inaamini kuwa uandishi wa habari unaotumia takwimu na ushahidi ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha masuala yanayogusa maisha ya wananchi yanapata nafasi inayostahili katika mijadala ya umma na michakato ya kufanya maamuzi.
Kupitia Tuzo hizi, tunawahimiza waandishi wa habari kutoka Unguja na Pemba kutumia kalamu zao, takwimu na ushahidi katika kuibua masuala yenye umuhimu kwa jamii na kuchangia Zanzibar yenye uelewa, uwajibikaji na maendeleo jumuishi.
