
WAANDISHI WA HABARI WAHIMIZWA KUANDIKA HABARI ZA HAKI YA AFYA YA UZAZI
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt. Mzuri Issa Ali, amewataka waandishi wa habari kuandika habari zinazohusu haki ya afya ya uzazi ili kuhamasisha jamii kuwa na uzazi salama na kizazi chenye afya bora.
Akifungua mafunzo ya siku mbili kuhusu haki ya afya ya uzazi kwa waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari kutoka Unguja, kwa niaba ya Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Afisa Rasilimali Watu wa TAMWA ZNZ, Tatu Ali Mtumwa, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuandika habari zitakazotoa uelewa kwa jamii kuhusu haki ya afya ya uzazi. Pia, amesisitiza umuhimu wa kuondoa dhana potofu kuwa afya ya uzazi inahusiana tu na ujauzito, kujifungua na kunyonyesha.
“Mafunzo haya ni chachu ya uchechemuzi na ukombozi wa jamii kupitia elimu inayotolewa na vyombo vya habari. Yanawezesha jamii kufuatilia na kuelewa afya ya uzazi katika kila hatua ya maisha.,” amesema Tatu Ali Mtumwa.
Akiwasilisha mada kuhusu afya ya uzazi, Daktari Bingwa wa Maradhi ya Wanawake na Uzazi, Dkt. Ummulkulthum Omar, ameleza kuwa kabla ya kupata ujauzito, mwanamke anapaswa kuwa na afya njema ili aweze kubeba ujauzito na kujifungua salama, yeye na mtoto wake.
“Lishe bora, uchunguzi wa afya wa mara kwa mara, na ushiriki wa jinsia zote katika kulinda afya ya uzazi ni nguzo muhimu kwa kizazi chenye afya bora tangu utoto, ujana hadi uzee. Hali hii hupunguza hatari ya kupata magonjwa mbalimbali ya afya ya uzazi, ikiwemo kansa ya shingo ya kizazi na magonjwa ya kujamiiana” amesema Dkt. Ummulkulthum Omar.
Kwa upande wake, mwanaharakati wa afya ya uzazi, Sihaba Saadati, akiwasilisha mada kuhusu maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) amesema kuwa wanawake wanaofanya biashara ya ngono na wanaotumia dawa za kulevya wako kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU.
Naye, Mkufunzi wa habari na mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Imane Duwe, amesema kuwa umefika wakati kwa waandishi wa habari kuandika habari na makala zinazobeba uhalisia wa matukio na kueleza changamoto wanazopitia watu mbalimbali ili kuhakikisha matatizo ya afya ya uzazi, ikiwemo mimba za utotoni, magonjwa ya kuambukiza na lishe duni yanafikishwa kwa jamii kwa uwazi na kwa kina.
“Tuhakikishe tunatoa fursa kwa jamii kuibua changamoto wanazokabiliana nazo, kisha sisi kama wataalamu wa habari kuzichakata kwa mtiririko unaofaa, kwa kuzingatia maadili na taaluma ya uandishi wa habari,” amesema Imane Duwe.
Kwa upande wao, waandishi wa habari waliopata mafunzo hayo wamesema kuwa watafanyia kazi mafunzo hayo kwa ufanisi kwa kuibua changamoto zinazohusiana na afya ya uzazi na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa uzazi salama.
Mafunzo kwa waandishi wa habari yameandaliwa na TAMWA ZNZ kupitia program ya kutumia vyombo vya Habari kukuza haki ya afya ya uzazi kwa Wanawake na Wasichana wa Vijijini na Mijini.
MWISHO